Jumatano, 22 Agosti 2018

PESA KATIKA MDOMO WA SAMAKI

Andiko: Mathayo 17:24-27
“Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli? Akasema, Hutoa. Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru. Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kwamba hapa duniani, kila mtu anahitaji fedha kwaajili ya kutimiza mahitaji yake, Bila fedha wakati mwingine ni vigumu kukidhi mahitaji yetu yote,kwa kadiri siku zinavyokwenda na hali ya uchumi inabadilika na kwa sababu hiyo fedha inazidi kuwa ngumu sana, na maisha yanabadilika mno na kwa sababu hiyo fedha zinahitajika ili wana wa Mungu wasiweze kukudhalilisha, kutokana na kukosekana kwa fedha,
Yesu anatoa suluhu namna ya kupata fedha katika muujiza huu
Muujiza wa Yesu, kumtuma Petro kuvua samaki na kupata fedha unaonekana kutajwa katika Injili ya Mathayo pekee, penginepo kwa vile yeye alikuwa mtoza ushuru, ingawa watoza ushuru hawa hawakuwa mawakili ya serikali ya Rumi bali walikuwa watoza ushuru kwaajili ya ujenzi wa Hekalu.
Watoza ushuru wa Hekalu walimuuliza Petro kama Mwalimu nwao analipa kodi ya hekalu nae aliwajibu kuwa analipa,Petro aliporejea Yesu alizungumza naye kuhusu swala aliloulizwa kuhusu kodi
“Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru .” Yesu alikuwa akimaanisha wao kama wana wa Mungu wako huru wasingelipaswa kulipa kodi ile, lakini ili aiwakwaze watoza ushuru, Yesu alitoa maagizo kwa Petro nini anapaswa kufanya ili kukidhi hitaji hilo la kulipa kodi, tunaona Yesu akimuelekeza Petro kwenda kutupa Ndoana na kuvua samaki na samaki yule wa Kwanza angekuwa na fedha ambayo ingetosha kulipa Kodi yake na Petro. Watu wengi na walimu wengi wa neno la Mungu hawasemi mengi kuhusu muujiza huu,
Lakini mimi naona yako mambo ya kujifunza katika muujiza huu
1. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali tuliyonayo katika Maisha
2. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya kumuabudu Mungu na kumtumikia
3. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya kulipia ada za shule za vijana wetu
4. Wote tunahitaji fedha kwaajili ya hatima ya wale wanaotuzunguka na wanaotutegemea
5. Wote tunahitaji fedha kwaaji ya kujiwekea hadhina mbinguni, tunapomtolea yeye na kuwapa wajane na masikini, na kutunza wazee wetu, na kuukuza ufalme wa Mungu.
Kama Petro na Mwalimu wake hawangelipa Kodi hii wangedhalilika, watu wangemsema Yesu, kuwa anajifanya mtu wa Mungu lakini halipi kodi ya Hekalu, hivyo Yesu anatambua kuwa watoto wake wanapokosa fedha wanadhalilika, wanaingia katika fadhaa, na hivyo alimuelekeza Petro nini cha kufanya.
Yesu alifanya Muujiza huu kuonyesha kuwa ana nguvu dhidi ya Fedha, “Jesus Has power over money” Yeye anauwezo juu ya fedha, Tatizo kubwa la watu wengi wa Mungu leo hawajawahi kumuambia Yesu kuwa wanashida ya fedha, linapokuja tatizo la fedha haraka sana hapo ndipo watu wengi sana hutumia akili na kuanza kusugua vichwa vyao, sio tu kusugua vichwa pia huanza kuumia moyo, na kuingia hofu na hata kulalamika, Tumesahau kabisa kuwa Mungu wetu anauwezo wa kutusaidia kama alivyomfanyia Petro .
Ni muhimu kufahamu kuwa Yesu ana uwezo juu ya fedha, Biblia inaeleza wazi kuwa yeye ingawa alikuwa tajiri alifanyika Masikini ili sisi tuwe matajiri 2Wakoritho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”
Biblia inatufundisha kuwa ni yeye anayetupa nguvu ya kupata utajiri Kumbukumbu 8:18 “Bali utamkumbuka Bwana, Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri; ili alifanye imara agano lake alilowapa baba zako, kama hivi leo.”
Biblia inaonyesha kuwa Petro alikuwa na uhitaji na hivyo huenda alimtaarifu Yesu kilichotokea, kwa ufupi alimuomba, kuhusu uhitaji wa kulipa kodi kwamba wanadaiwa kodi, na Yesu alijibu maombi hayo, kwa msingi huo kama tunavyoomba kwaajili ya mahitaji mengine tunahitaji pia kumuomba Mungu atupe fedha ili tusidhalilike.
Biblia inasema Hamna kitu kwa sababu hamwombi ni lazima tumuombe Mungu kwaajili ya hali ya uchumi wa familia zetu na mahitaji yetu, Sala ya Bwana inasema utupe leo riziki yatu ya kila siku, riziki yetu ya kila siku haiwezi kupatikana bila kuhusisha fedha je tumewahi kuomba fedha?
labda wengi tumefungwa na ile dhana ya fundisho la shina la mabaya yote ni kupenda fedha, lakini biblia inamaanisha kupenda fedha kuliko Mungu, na haimaanishi kuwa watu wake hawahitaji fedha, hapa mimi nazungumzia ule uhitaji fedha wa kawaida, kama ilivyokuwa kwa Petro anadaiwa kodi, labda huenda na wewe unadaiwa kodi ya nyumba, ama una madeni, ama unadaiwa ada ya watoto wako na kadhalika haja za namna hii ni vema pia Mungu akazijua, wengi hunijia wakitaka maombezi ya namna mbalimbali, lakini sijawahi ona mtu akinijia kuomba maombi apate fedha, wengi linapokuja swala la uhitaji wa kifedha, wanatumia akili zao wenyewe na wanaishia kupata msongo wa mawazo, huku haja hiyo ikiwa haijawasilishwa kwa Mungu, kutokumwambia Mungu uhitaji wetu wa kifedha ni daharau, ni sawa na kufikiri kuwa labda swala la kupata fedha Mungu haliwezi, lakini maandiko yanasemaje yote yawezekana kwa Mungu. kwa nini unasumbuka hali neno la Mungu linasema
Wafilipi 4: 6 maandiko yanasema “ Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.”
Je umewahi kumuomba Mungu waziwazi kwamba akupatie fedha ? umewahi kumuombea Mumeo, mkeo, wazazi, ndugu zako wawe na upenyo wa kifedha? Lazima tumuombe Mungu katika hitaji hili.
Mathayo 7: 7-11 Biblia inatukumbusha kuwa, Mungu ni Baba mwenye upendo ambaye huwapa watoto wake Mahitaji kwa kadri walivyoomba.
Anauliza je ni nani kati yenu mwanaye akiomba mkate atampa Jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka? Nauliza umewahi kumuomba Mungu akupe fedha ? au umetamani tu kuwa na fedha kwa kutumia akili zako mwenyewe bila kumwambia Mungu
Anamalizia kwa kusema " kama ninyi mlio waovu mwaweza kuwapa watoto wenu vipawa vyema je si zaidi sana Baba yenu Wa Mbinguni .........'' Hivyo kile tunachokiomba ndicho tutakachopokea.
1 Petro 5: 7 maandio yanasema wazi kuwa, Mungu hujishughulisha Zaidi na Mambo Yetu na hivyo tumpe yeye Fadhaa/haja zetu.
Anasema.
7 huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.
Kama utasema hujui namna ya kuomba hususani kuomba fedha kwa Mungu basi fuata muongozo wa mambo ya kuombea:-
Mambo ya kuombea:
• Omba Mungu akuweke mbali na Madeni, Yesu na Petro hapa walikuwa wanadaiwa kodi ya hekalu. na petro alipatwa na fadhaa
• Omba Mungu akusaidie usiwe mzigo kwa wazazi wako
• Omba Mungu kwamba akupe fedha nyingi kuliko matumizi
• Omba Mungu kwamba uwe na uwezo wa kukopesha na sio kukopa
• Vunja roho ya umasikini, kataa mikosi inayoendana na kipato chako
• Kataa roho ya umasikini na magonjwa na masumbufu
• Kemea Roho za wizi, hasara, mikosi, chuma ulete, kukopera na jicho baya, Mwambie Mungu akupatie ulinzi wa kutoshja katika mali zako.
Mwambie Mungu atumie ujuzi aliokupa au atakaokupa kukupa fedha
Yesu alitumia ujuzi aliokuwa nao Petro, kumpatia fedha, Petro alikuwa Mvuvi kabla ya kumtumikia Mungu, kwa kuwa mwanafunzi wa Yesu. Hivyo Yesu alitumia ujuzi na kipawa alichokuwa nacho ili kupata fedha ya kulipa kodi. alimuagiza aende akavue samaki na muujiza ulikuwa ndani ya samaki wa kwanza atakayevuliwa, kumbe fedha zetu ziko katika midomo ya samaki, ni lazima twende kwenye ujuzi ule tulionao tuweze kuzitoa fedha zetu huko na kukidhi mahitaji yetu tuliyo nayo
Fanya kazi kwa bidii, ile kazi aliyokupa Mungu fanya kwa uaminifu, fanya kama unamtumikia Mungu yeye anasema atazibariki kazi za mikono yako.
Yesu hakumwambia Petro akacheze Biko wala tatu mzuka hii ni michezo ya watu waliokata tamaa, wanaishi kwa kubahatisha, ni michezo ya watu masikini, wanaoishi kwa ndoto za mchana, wakitarajia kitu kutoka kwa miungu ya bahati nasibu, Mungu hajatuleta duniani ili tuishi maisha ya kubahatisha kanuni kuu za mafanikio ziko katika kazi naujuzi au kipawa ulichopewa na Mungu huko ndioko pesa yako iliko,
Biblia inatutaka tufanye kazi kwa bidii, Pesa iko katika mdomo wa samaki. Lakini ni lazima ukavue, ukienda kuvua samaki yule utakayemvua ana pesa mdomoni mwake, za kukidhi mahitaji yako ya ya jamaa zako, Nikutakie uwajibikaji mwema na Mungu aibariki kazi ya mikono yako Amen. Nakukumbusha kuwa fedha yako iko katika midomo ya samaki endenda ukatupe ndoana.

BWANA YU KARIBU NA WALIOVUNJIKA MOYO, NA WALIOPONDEKA ROHO HUWAOKOA.

Andiko la msingi: Zaburi 34:17-19 “ Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”
"Bwana yu Karibu na Waliovunjika Moyo, Na waliopondeka Roho Huwaokoa Zaburi 34:18"
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa tuwapo duniani wanadamu tunazungukwa na changamoto nyingi, kwa kawaida Mungu ameruhusu tuweze kupitia nchangamoto za aina mbalimbali kwa makusudi mbalimbali, aidha ya kutufundisha ama kutufanya tukue kiroho, kihekima na kimaadili lakini wakati mwingine kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, hata hivyo wakati tunapopitia changamoto hizo, mara kadhaa wanadamu huwa tunakata tamaa, na tunaweza kujiuliza kama hivi Mungu anaona kweli? Hivi Mungu yupo? Kama yupo kwa nini anaachia jambo kama hili, kwa nini hakuzuia, kwa nini hakunitahadharisha mapema? Mbona yuko kimya Hivi yeye yupo kweli?tunaweza kufikiri kuwa Mungu ametuacha.
Katika nyakati hizi ngumu ndio nyakati ambazo ni rahisi kumuwazia Mungu kwa upumbavu, yaani kumfikiria Mungu kwa namna isiyofaa,Watakatifu waliotutangulia waliokuwa na ujuzi kuhusu Mungu walifahamu kuwa wanadamu wana changamoto nyingi maandi yanasema hivi kupitia Ayubu;-
Ayubu 14: 1 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. ”
Wote tunafahamu jinsi Ayubu alivyopitia majaribu na mateso Magumu lakini Biblia inatuambia kuwa Ayubu katika dhiki yake hakuwahi kumkufuru Mungu wala kumuwazia Mungu kwa upumbavu,
Ayubu 1:20-22 “ Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu .”
Hali kama hii ndio iliyomtokea mwandishi wa Zaburi hii, kwa mujibu wa masimulizi ya tamaduni za kiyahudi Zaburi hii imethibitika kuwa iliandikwa na Daudi, au moja ya viongozi wa kwaya wa Daudi, na mazingira ya uandishi wa zaburi hii ulitokana na tukio la Daudi kunusurika katika hatari mbaya iliyokuwa ikimkabili, Zaburi hii iliandikwa mara baada au kwa kusudi la kukumbuka namna Daudi alivyonusurika katika hatari ngumu katikati ya mfalme wa wafilisti alipokuwa akitafutwa na Sauli ili aweze kuuawa Katika Mazingira haya magumu Daudi aliweza kujifanya mwendawazimu ili kupata namna ya kuondoka mikononi kwa Akishi mfalme wa wafilisti.
1Samuel 21:10-15 “Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,Sauli amewaua elfu zake,Na Daudi makumi elfu yake. Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakuna-kuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mwaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe hiki ili aonyeshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu? ”
Ni katima Mazingira ya aina hii ndio Daudi alipoimba zaburi hii ya 34 akzizungumza maneno ya kushangaza sana hata baada ya tukio hili gumu namna hii Daudi aliweza kumsifu Mungu, alionyesha kuwa Mungu ni tumaini lake, hakutaka kulalamika alitaka watu wote wawe wanyenyekevu wamtumaini Mungu wamweleze shida zao na kuwa yeye atawaitikia kwa kuwa Ni Mungu aliye karibu na watu wake angalia maneno yake hiyo isiyo ndefu sana Zaburi 34:1-22
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati, Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
2. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
3. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
4. Nalimtafuta Bwana akanijibu, Akaniponya na hofu zangu zote.
5. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, Wala nyuso zao hazitaona haya.
6. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote.
7. Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
8. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.
9. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.
10. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa; Bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu cho chote kilicho chema.
11. Njoni, enyi wana, mnisikilize, Nami nitawafundisha kumcha Bwana.
12. Ni nani mtu yule apendezwaye na uzima, Apendaye siku nyingi apate kuona mema?
13. Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila.
14. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.
15. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao.
16. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
17. Walilia, naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote.
18. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.
19. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.
20. Huihifadhi mifupa yake yote, Haukuvunjika hata mmoja.
21. Uovu utamwua asiye haki, Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.
22. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao.
Unaweza kuona hatupaswi kukata tamaa wala kuvunjika Moyo katika mazingira yoyote, katika hali Ngumu zinazotukabili Mungu na aendelee kuwa Mungu wetu, tusimuwazie kwa Upumbavu tuendelee kuuona mkono wake, na kumtegemea yeye katika hali zozote, tusinungunike, bali afadhali kumlilia yeye,
Manunguniko yanaondoa Baraka za Mungu, Manunguniko, yanamkasirisha sana Mungu, badala ya kulalamika na kunung’unika ni afadhali kumlilia yeye na kumhimidi yeye Daudi anasema atamhimidi Bwana kila wakati maana yake katika hali yoyote na Mungu yu Karibu na waliovunjika moyo na wanaonyenyekea kwake yeye huwakomboa huwahurumia na kuitikia kilio chao.
Mungu aitikie kilio chako Ndugu yangu, Mungu na awe karibu nawe Mungu asikupungukie Mungu asikufanye ukufuru Usivunjike moyo, wakati unapopita katika Magumu, Mungu yuko Karibu, Mungu hajatutupa wala hajakutupa wewe anakujali yuko Karibu nawe mtafute wakati huu wa dhiki yako atakutokea nawe utasadiki ya kuwa Mungu amenituma nikuhakikishie kuwa Yuko Karibu nawe Bila shaka atakufuta Machozi yako leo, BWANA YU KARIBU NA WALIOVUNJIKA MOYO, NA WALIOPONDEKA ROHO HUWAOKOA.

FURAHA TIMILIFU

Mstari wa Msingi: Yohana 16: 23 -24 “ Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; FURAHA YENU IWE TIMILIFU .”
Je wewe hutegemea hali ya nje kama chanzo cha Furaha maishani mwako? Angalia kwamba Mungu ndio chanzo kikubwa cha furaha timilifu na sio vinginevyo
Utangulizi:
Maisha ya mwanadamu yanategemea sana kuwa na furaha ili yawe maisha, na mwanadamu siku zote anafanya kila kitu kwaajili ya furaha yake tuu. Furaha ndio kilele cha maisha ya mwanadamu, kila analolifanya mwanadamu lengo lake kuu ni kupata furaha.
Mathalani ukitoa msaada kwa mtu moyo huwa na furaha, ukipongezwa au kusifiwa kwa jambo fulani moyo huwa na furaha, ukiwa mshika ibada moyo huwa na furaha, ukiwa na mke mwema au mume mwema moyo huwa na furaha vilevile, ukiwa na watoto wazuri na wenye adabu na kujiheshimu, ukifanya kazi kwa ufanisi, ukipata malipo ya kazi yako au mshahara moyo huwa na furaha kadhalika, ukisikiliza mziki au filam ama picha na hata kusoma vitabu moyo huwa na furaha pia, Ukiwa na mafanikio makubwa, ukijenga nyumba, ukiwa na mashamba, ukinunua gari, ukipandishwa cheo, ukichumbiwa, ukiolewa, ukizaa mtoto, ukiwa na afya njema moyo huwa na furaha, ukipewa tuzo, ukishinda uchaguzi, ukimiliki kampuni na kufanikiwa Moyo huwa na furaha Lakini pamoja na hayo yooote bado utaweza kuona kuwa hakuna furaha iliyo timilifu, Je ni wapi tunaweza kuona na kuwa na furaha timilifu?
Furaha nini?
Ni vigumu sana kuielezea furaha zaidi ya neno lenyewe furaha, Katika kiingereza neno linalotumika kuelezea furaha ni “ JOY ” ambalo katika lugha ya kiyunani ni “ CHARA ” linatamkwa “KHA-RAH ” ambalo maana yake ni Hali ya kujaa raha katika nafsi kutokana na kufikia au kufanikiwa katika jambo fulani, hali ya kuwa na raha isiyo na mipaka kutokana na kutoshelezwa kwa nafsi.
Katika imani ya Kikristo tunaweza kusema ni Raha ya nafsi ndani ya mwamini anayopipata kama matokeo ya Neema na upendo wa Roho Mtakatifu kumuwezesha mtu huyo, kufurahia kuwa na uhusiano na Mungu na kumjua Yesu Kristo, Neno lake na makusudi yake na tumaini lililo ndani yake.
Je ni watu wangapi wana furaha?
Ukiulizwa swali je una furaha je unaweza kulijibu vipi? Ni swali gumu sana, kwani unaweza ukawa una furaha lakini unafahamu kuwa furaha hiyo haidumu milele. Labda una furaha kutokana na kuwa una familia nzuri, lakini kwa kina utaona kuwa furaha hiyo inategemea uwepo wa familia nzuri, na uwepo huo ukitenganishwa kwa vifo, maisha, mabadiliko mbalimbali basi furaha yake nayo inaisha. Hivyo kuna furaha za milele na furaha ya muda mfupi.
Kila mtu anapenda kuwa na furaha, na lengo kuu la maisha ni kuwa na furaha. Hata hivyo furaha ya watu wengi sana sio furaha timilifu kwa sababu furaha zao zinatawaliwa na hali ya nje ya maisha yao angalia mfano huu:-
Mtu moja alikuwa anamiliki nyumba nzuri sana ni nyumba ya thamani na ilikuwa yenye kupendeza na yenye mvuto mkubwa sana katika mji aliokuwa anaishi, na jamaa huyu aliipenda nyumba yake sana watu wengi waliwahi kumuendea na kumuomba awauzie hata kwa bei kubwa mara mbili ya thamani yake lakini alikataa, wakati fulani bwana huyu alisafiri na aliporejea aliikuta nyumba yake ikiwa inawaka moto mkubwa sana na hivyo alipatwa na huzuni kubwa mno! Mamia ya watu walikusanyika kwaajili ya kuangalia namna ya kusaidia kuuzima moto ule, lakini hakuna walichofanikiwa kukiokoa katika moto ule
Mara mwanae mkubwa alimjia na kumnongoneza sikioni, Baba usiogope, “Niliiuza nyumba hii jana na niliiuza kwa bei nzuri sana, bei ilikuwa nzuri kiasi ambacho nisingeliweza kukusubiri au kukutaarifu, Hivyo unisamehe bure tu baba”
Baba yule alivuta pumzi na kuzishusha akimshukuru Mungu kwani sasa amekuwa moja ya washuhudiaji wa ajali ile kama walivyo wengine,
Mara mwanae wa pili alikuja mbio akimkimbilia na kumbwambia baba unafanya nini uangalia nyumba yetu ikiwa inaungua? Baba alimjibu kijana yule kuwa tulia kwani kaka yako aliiuza tayari kwa bei nzuri, Kija ayule alimwambia baba yake kuwa tulichukua kiwango fulani tu cha fedha na sio zote hivyo nina mashaka kama yule aliyenunua atakubali kumalizia ilihali nyumba imeungua!
Yule baba alianza kulia tena, machozi ambayo mwanzoni alikuwa ameshasahau,Moyo wake ulianza kwenda mbio sana na nguvu zikaanza kumuishia alikuwa mwenye huzini kubwa sana, Mara mtoto wake wa tatu akaja na kumwambie Baba yule mtu aliyenunua nyumba yetu ni mtu mwema na mwaminifu na mwenye kutunza sana ahadi kwani nimetoka kuongea naye sasa na ameniambia “ Haijalishi kwamba nyumba imeungua au la Nyumba ni yangu na nitalipa kiwango chote cha fedha tulichopatana, kwa kuwa hakuna aliyejua kuwa nyumba itaungua, Kisha wote wakasimama wakiwa wametulia kama washuhudiaji wengine wakiangalia nyumba inayoungua bila wasiwasi wowote!
Tunajifunza nini kutokana na kisa hiki? Watu wengi sana wanajisikia kuwa wenye furaha kutokana na hali ya nje ya mambo na sio ya ndani na kwa sababu hiyo hawawezi kuwa na furaha ya kweli, furaha ya kibinadamu ya ya dunia hii ni yenye kuyumba kutokana na hali halisi ya kubadilika badilika kwa mambo, aidha furaha ya kweli haipatikani kwa kuwakosea wengine.
Wako watu wengine wanafikiri kuwa watakuwa wenye furaha kwa sababu ya kukandamiza wengine, kuwatesa, kuwatendea vibaya, kuwashitaki, kuwasengenya, na kuwakosea ni muhimu kufahamu kuwa watu wote wanahitaji furaha kwa sababu hiyo kama huwezi kuwasaidia wengine kuwa wenye furaha basi jitahidi usiwe sababu ya huzuni zao, furaha ya kweli hua kwa kuhakikisha kuwa wengine wana furaha kama wewe na sio kuwakosea.
Faida za kuwa na furaha timilifu
Kwa mujibu wa wataalamu wa maswala ya saikolojia wanaeleza kuwa furaha ina faida kubwa sana
Zikiwemo
a. Inakulinda na magonjwa ya Moyo
b. Inaimarisha kinga za mwili
c. Inatupilia nje mikandamizo ya mawazo katika maisha
d. Inakulinda dhidi ya Magonjwa
e. Inarefusha maisha
Kitaalamu hata utungiswaji wa Mimba hutokea siku ambayo wana ndoa wote wamefurahi
Unawezaje kuwa na Furaha timilifu?
Kaa katika uwepo wa Mungu Zaburi 16:11 “Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso wako ziko furaha tele; Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.” Unaweza kuona maneno Mbele za uso wako ziko furaha tele yanamaanisha mbele za uwepo wa Mungu “ Presence” kuna furaha tele, Musa alikuwa ni mtu aliyependa kukaa katika uwepo wa Mungu, alikaa uweponi mwa Munngu kiasi ambacho hakusikia njaa kwa siku 40 na hata aliporejea uso wake ulikuwa unangaa’ kiasi ambacho watu walishindwa kumtazama Kutoka 34:29-35 “ Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo BWANA amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za BWANA kusema naye, kuuvua huo utaji mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling'aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena, hata alipoingia kusema naye.”
Usitawaliwe na hali ya nje.
Habakuki 3:17-18 “ Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe; Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.” Kwa mujibu wa Habakuki ni kuwa yeye atamfurahi Mungu bila kujali kuwa mtini haujachanua maua, au zabibu hazina matunda aku mzaituni haukuzaa au mashamba hayakutoa chakula au mazizi mifugo kutokuwa na kitu, Yeye bado atafurahi, hii ni wazi kuwa Mungu ndio chanzo cha furaha yetu na sio vinginevyo.
Dumu katika kuomba.
Kwa mujibu wa Yesu Kristo ukweli ni kuwa maombi yanasaidia kwa kiwango kikubwa sana kuketa firaha timilifu, kila amtu anapaswa kuomba, maombi ni muhimu sana, usiache kuomba Yohana 16: 23 -24 “Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; FURAHA YENU IWE TIMILIFU .”
Mwamini Mungu na Kumtegemea.
Warumi 15:13 “Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu. ”, Imani katika Mungu na kumtegemea yeye kunaweza kutupa furaha timilifu.
Watumikie wengine Watu wanaowatumikia wengine huwa na furaha sana Duniani.
Na Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumanne, 21 Agosti 2018

KUFUFUKA KWA YESU


KUFUFUKA KWA YESU. 
  =Yesu baada ya kukaa kwenye uso wa nchi huku akishughulika kuhakikisha wokovu unapatikana kwa watu wote watakao mwamini kama tulivyoona baadhi ya mambo muhimu Yesu aliyoyafanya kwenye ulimwengu wa roho, hatimaye siku ya tatu alifufuka.
=iyo tu kwamba alifufuka lakini yuko hai milele na milele na mauti haina nguvu juu yake tena,
=Yesu ni mwanadamu pekee hadi leo ambaye kaburi lake liko wazi, kwa sababu kama ni kufufuka tu siyo hoja, kuna watu wengi katika historia walifufuka lakini baada ya muda walikufa tena.
=Kufufuka kwa Yesu kuna umuhimu gani kwetu?
=Siwezi kwa leo nikaelezea mambo yote yaliyotokea ya ajabu kwa sababu ya Yesu kufufuka, lakini labda nikuoneshe kitu hapa;
=Kwanza kabisa imani yetu ina nguvu sana kwa sababu Yesu japo alikufa lakini alifufuka na akawa hai milele na milele.
=Yaani kama Yesu asingalifufuka imani yetu ingekuwa bure na asingekuwa na utofauti na waanzilishi wa dini zilizopo hapa duniani tunazozifahamu kama Muhamedi wa dini ya kiislamu na wengineo ambao hata sasa bado wamelala makaburini.
=Hebu angalia hii:
1Wakor 15;14 *“tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure”
Isitoshe hapo chini kwa msisitizo ikarudiwa;*
1Wakor 15;17 ” Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu”
=Yesu alipofufuka ni nini kilitokea?
=Jambo kubwa sana lilitokea kiroho kwa sababu kwa kufufuka kwake aliishinda mauti ambayo ndiyo ilikuwa inafanya kazi kwenye maisha ya mwanadamu kwa sababu ya dhambi.
=Tena mauti ninayoiongelea hapa ni mauti ya kiroho ambayo ni kutengwa na Mungu milele.
=Kwa hiyo mwili wake ulifanyika limbuko (mzaliwa wa kwanza) kwa ajili ya wote wanaomwamini Yesu kwa hata wakipatwa na mauti ya kimwili lakini bado watafufuliwa tena na kuvikwa miili ya mbinguni na waishi milele na milele kama mwokozi wao.
1Wakor 15:20-23 “Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala. Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa. Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja”
=Kama unakumbuka tuliona kwamba Yesu pia anaitwa mzaliwa wa kwanza wa waliyokufa, ikimaanisha kwamba yeye ndiye mtangulizi kwa ajili ya wengi waliyokufa katika yeye kwamba siku moja nao watafufuka kama yeye.
=Hebu angalia tena hapa;
1Wakor 15:55-57 “Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo”
=Kuna mambo mengi sana hapa ya kujifunza na ninajua tutaendelea kuyaona zaidi, lakini kwa sasa angalau uwe na haya maarifa na taarifa hizi zikusaidie kujua mambo yaliyotendeka siku ulipookoka na wewe ambaye hujaokoka bado Bwana ana haja nawe tafadhali kama ukiwa tayari nione inbox au mwone mtumishi yeyote wa Mungu unayemwamini akusaidie.

KAZI YA YESU YA WOKOVU.


=Mungu wangu aendelee kukubariki sana kwa kuendelea kuwa mfuatiliaji mzuri wa masomo haya ambayo bado tunayo safari nzuri tu ya kuendelea kujifunza siri hizi za ufalme wa Mungu.

=Bado tupo kwenye eneo hili la kazi ya Yesu ya wokovu, tukiwa mwishoni mwishoni kabisa ninaamini Bwana ni mwema kwa ajili yetu anachotaka tukijue safari hii lazima tukipate hakika.

=Kipindi kilichopita tulipata nafasi ya kuangalia eneo kidogo tu kuhusu kifo cha Yesu, kwamba kwanini ilibidi kiwe cha msalaba na sii vinginevyo.

=Leo nataka tuangalie kuzikwa kwake na kukaa kaburini siku tatu na mwishowe kufufuka, kuna siri kubwa hapo.
 *KUZIKWA KWAKE.*
=Kimsingi siongelei kile kitendo cha kuzikwa bali ninaongelea ule muda tangu aisalimu roho yake hadi alipofufuka siku ya tatu kama alivyosema.

=Kwanza kabisa niweke sawa hapa, Yesu hakukata roho bali aliitoa/aliisalimu roho yake, kwa maana kwamba Yesu kwa sababu ni Mungu hakuna mwanadamu ambaye angeweza kumwondoa uhai wake lakini alikubali mwenyewe kuutoa kisha akaja kuurudisha tena.

=Japo ukisoma kwenye tafsiri yetu ya Kiswahili injili ya Marko na Luka waliandika kwamba alikata Roho, lakini ukienda kwenye tafsiri za awali za biblia ya King James old version inasema wazi kwamba aliitoa roho yake na siyo kukata Roho.

=Injili ya mathayo na Yohana yenyewe ilitafisiriwa vizuri hilo neno; Mathayo alitimia neno kutoa uhai, la Yohana ametumia neno kuisalimu Roho, ambazo zote hizo zimekaa vizuri kama tafsiri za awali zilivyo.

=Hebu angalia hapa;
Yoh 10:17-18 *“Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu”*

=Ninaamini tuko sawa mpaka hapo.

=Sasa kilitokea nini katika ulimwengu wa roho wakati Yesu akiwa amekufa?

#Kwanza kabisa, kuanzia saa sita hadi saa tisa kabla Yesu hajaitoa roho yake kulikuwa na giza nchi yote maandiko yanasema hivyo; hiyo ilikuwa ni ishara kama ulimwengu wa giza umeshinda lakini dakika chache baadaye baada ya Yesu kuitoa Roho yake wakatu huo huo;

@tetemeko kubwa likatokea juu ya nchi,
@miamba ikapasuka,
@pazia la hekelu likapasuka kuoka juu hadi chini
@na cha kushangaza zaidi miili ya watakatifu wa kale waliyokuwa wamekufa wakafufuka tena wakawatokea wengi huko Yerusalemu.

=Hebu angalia maandiko;
Mathayo 27:50-53 *“Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi”*

=Siwezi nikaelezea kila kitu lakini nimelenga zaidi kwenye pazia kupasuka la kupaingia patakatifu hadi patakatifu pa patatakatifu, hapa ilikuwa inaonyesha sasa kwamba njia iko wazi kwa kila mmoja atakayeoshwa nah ii damu ya Yesu kuingia patakatifu kwa sababu naye ni kuhani.

=Lakini pia ilionesha kwamba Yesu aliye kuhani mkuu aliingia na damu yake mwenyewe hadi patakatifu pa patakatifu na kuinyunyizia kwenye kiti cha rehema ili kufanya upatanisho wa Mungu na manadamu wote watakao mpokea.
 Haya yalifanyika ndani ya hizi siku tatu Yesu akiwa kwenye uso wa nchi kama maandiko yasemavyo;

2Wakor 5:19 *yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.*

=Kuna kitu kingine cha ajabu hapa; mwanzoni kabla Yesu hajafa watu wote waliyokuwa wanakufa walikuwa wanaenda sehemu moja iliyokuwa imetenganishwa iliyoitwa kuzimu ambayo hadi sasa kuzimu ipo na ndiyo makao ya shetani na roho zote ovu pamoja na roho za wanadamu waliyokufa katika dhambi.

=Kabla ya Yesu ilikuwa kwamba ukifa mcha Mungu unaenda mahali palipoitwa kifuani mwa Ibrahimu ambako hakuna mateso badala yake ni raha tu, kulikuwa na shimo kubwa lililowatenga ambapo upande wa pili ndipo kuzimu kwenyewe ambako roho za wenye dhambi huenda kuteseka wakisubiri hukumu ya mwisho.

=Ndiyo maana kama unakumbuka Yesu alitoa mfano wa Tajiri na Lazaro namna walivyoishi duniani na maisha yao baada ya haya ya duniani.

=Sina muda lakini naomba usome kwa utulivu LUKA 16:19-31, *utakutana na kisa hiki. Ndiyo hali halisi ilivyokuwa kabla ya Yesu hajafa.*

=Ni nini kilitokea Yesu alipokufa?

=Tumesoma hapo kwamba miili ya watakatifu iliinuka kutoka makaburini tena hata hao waliyofufuka wakawatokea watu na kuuingia mji mtakatifu yaani Yerusalemu.

=Yesu naye alipokufa kama mwanadamu wa kawaida roho yake ilishuka kuzimu, na alipofika kuzimu kwenye eneo la wenye haki au watakatifu kama naye alivyokuwa mtakatifu akawatoa wote kuzimu ili awahamishie makao yao, ndiyo maana biblia inasema ilifufuka miili ya watakatifu peke yao.

=Ndiyo akaihamishia mahali pengine paitwapo paradiso ambapo ni juu wala siyo mbinguni lakini ni mahali pa raha ambapo watakatifu wanapokufa wanaishi hapo wakisubiria kufunuliwa kwa Yesu mara ya pili.

=Ndipo akaenda upande wa pili wa kuzimu ambapo ndipo makao ya shatani na roho za wanadamu waatenda dhambi waliyokufa ambako pia kuzimu maana yake ni kifungoni, na Yesu akaenda kuwahubiria huko siyo ili waokoke bali akawaeleza kwamba yeye ndiye aliyekuwa anahubiriwa na manabii na torati.

=Najua unashangaa hii hujawahi kuishikia lakini nakufundisha biblia, hebu angalia hii;

1Petro 3:18-20 *“Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni (kuzimu), akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji”*

=Lakini baada ya hapo akamfuata Shetani ndipo akamnyang’anya ufunguo wa mauti na kuzimu, ikimaanisha sasa mauti haina nguvu wala kuzimu kwa wale wote wanaomwamini Yesu.

=Hizi ni siri za ndani kabisa ningeweza kukueleza mengi zaidi lakini Bwana atatupa wakati mwingine kuyachambua haya, hii nimekupa ili ikupe ujasiri na kujijua nafasi yako ilivyo ya thamani katika Kristo Yesu wewe uliyeokoka na kama bado nakupa nafasi kabisa unifuate inbox nitakuongoza vyema tena nitakuwa tayari kukusimamie hadi ukuo kiroho.

Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako. (KUM. 22:5 SUV).


Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume, wala mwanamume asivae mavazi ya mwanamke; kwa maana kila afanyaye mambo hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako. (KUM. 22:5 SUV).

Nimeonelea niongelee kidogo hili andiko ambalo sisi wahubiri tunalitumia sana kuwahukumu nalo wanawake katika uvaaji wao na kuwafanya wajisikie hatia sana.
Ili kuweza kulitafsiri andiko kiusahihi kwa ajili ya nyakati zetu lazima kwanza tujue linasema nini na lilikuwa lina maana gani kwa nyakati ambazo liliandikwa.
Anasema wazi mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume na mwanamume asivae mavazi ya mwanamke.
Hili andiko halisemi kuwa mwanamke asivae mavazi yanayofanana na ya mwanamume.
Katika siku za andiko hili mavazi ya wanaume na ya wanawake yalikuwa yanafanana kwa sehemu.
Ya kiume yalikuwa yanajulikana kama kanzu au joho wakati ya mwanamke yalikuwa yanajulikana kama gauni.
Wanaume na wanawake walikuwa wanafunga vitambaa vichwani mwao lakini namna ambavyo wanaume walifunga ilikuwa ni tofauti na vile wanawake walivyokuwa wanafunga.
Kuchukua hili andiko na kudhani linamaanisha wanawake wasivae suruali na kaptura ni kutokuelewa kabisa hili andiko linasema nini.
Mashati ya kike yanaitwa blauzi na blauzi za kiume zinaitwa shati.
Kuna mavazi ya aina nyingi tu katika tamaduni mbalimbali ambazo za kiume na za kike zinafanana.
Mtu wa Mungu kuna suruali za kike na za kiume.
Kuna kaptura za kike na za kiume.
Tofauti yake ni katika namna zilivyoshonwa.
Mwanamke anapaswa kuvaa mavazi ya kumsitiri na ajiepushe kuvaa mavazi ya kikahaba ndicho mimi ninachoona katika maandiko.
Mwanamke anaweza akavaa sketi au gauni na bado vikawa havijamsitiri na akawa amevaa kaptura au suruali na zikawa zimemsitiri.
Wadogo zangu wanaishi katika nchi ambayo vazi la heshima la kiume ni sketi.
Ukishaona unachohubiri hakiwezi kufaa kwenye kila jamii ya wanadamu jua tu kuwa unachohubiri kiko na shida mahali.
Hakuna mahali katika maandiko ambapo mwanamke amekatazwa kuvaa suruali au kaptura.
Kwanza wakati wa maandiko haya mavazi hayakuwepo.
Cha muhimu hapa ni sisi kama watu waliyookoka tuwe na kiasi katika namna tunavyovaa.
Tusivae huku tukiwa tumeacha sehemu zetu nyeti wazi au tukiwa tumebana mpaka kuchora viungo vyetu nyeti bila kujali tumevaa mavazi gani maana wakati mwingine mdada anaweza akavaa suruali ambayo haijambana wala kumchora na mwingine akavaa sketi au gauni iliyombana na ambayo haijamsitiri lakini yule aliyevaa suruali akaonekana kakosea katika kuvaa.
Ukifundisha mtu kuwa suruali ni kwa mwanamke ni dhambi akaenda India akakuta suruali ni vazi la heshima kwa mwanamke unamjengea ndani yake kuwaza kusiko sahihi kuwa wahindi wote wanakosea katika kuvaa.
Ukimfundisha mtu kuvaa sketi ni dhambi kwa mwanamume akienda Scotland na kukuta vazi la heshima la mwanamume wa kiScotish ni sketi utamjengea namna isiyo sahihi ya kufikiri kuwa waScotish wote ni wadhambi.
Tujiepushe kufundisha mitazamo yetu tubaki tunalihubiri neno.
Mtu anayesema kuwa suruali ni vazi la kiume ameamua kuwa finyu sana katika mtazamo wake anataka kutulazimisha wote tuwe finyu katika kuwaza kwetu.
Huyu mtu atafika mahali ambapo watu wapo huru kuvaa suruali bila ya kujali jinsia na atauhukumu wokovu wao based on mavazi bila  ya kuzingatia maudhui na maana hasa ya maandiko anayotumia.
Tuache kutiana hatia kwa mitazamo yetu binafsi isiyo na uhusiano wowote na Neno la Mungu.
NI HIVYO TU YAANI.